Chama cha Soka Nchini Misri, EFA kimemteua Kocha wa zamani wa Al-Ahly, Hossam El-Badry kuwa Kocha mkuu mpya wa timu yao ya taifa.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 amechukua nafasi ya Javier Aguirre ambaye alitimuliwa baada Misri kuondoshwa katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika 2019 na Afrika Kusini katika hatua ya 16 Bora.
Hossam kibarua chake Cha kwanza, itakuwa ni mechi ya kuwania Kufuzu kwa fainali za AFCON 2021, huko Cameroon ambapo Misri itakuwa na Mechi Mbili za nyumbani dhidi ya Kenya na Togo katika mechi za kundi G wakiwa pamoja na Comoro.
Hossam El-Badry hapo awali aliwahi kuwa kocha Mkuu wa Timu ya taifa ya Misri chini ya umri wa miaka 23.
Kocha huyo alianza kazi yake ya ukocha kama meneja msaidizi wa mkufunzi wa Al Ahly, Manuel Jose Mwaka 2005 na kuwa kocha mkuu 2009 na vilabu Vingine alivyofundisha ni ENPPI ya hapo hapo Misri, Al-Ahly Tripoli ya Libya pamoja na Al Merreikh Kutoka Nchini Sudan.