Mahakama ya Rufani nchini Tanzania imetengua hukumu na amri ya Mahakama kuu ya kuzuia wakurugenzi wa halmashauri, manispaa na majiji kusimamia uchaguzi Mkuu kwa niaba ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).
Uamuzi huo umetolewa leo, na kuifanya Serikali kushinda rufaa ya ma DED kusimamia uchaguzi, hivyo basi wakurugenzi wanaruhusiwa kusimamia uchaguzi.
Serikali ilifikia hatua ya kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama kuu ambayo ilitolewa na jopo la majaji watatu, lililo batilisha kifungu cha 7(1) cha sheria ya uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Pia jopo hilo lilibatilisha kifungu cha 7 (3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Ikumbukwe kuwa uamuzi huu wa sasa wa Mahakama kuu umetokana na kesi iliyofunguliwa na mashirika ya wanaharakati kupitia kwa mwanachama wa chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, akitetewa na Wakili Fatma Karume.
Aidha leo Mahakama kuu imesikiliza pia maombi ya ACT – Wazalendo kujiunga katika kesi ya ukomo wa Urais. uamuzi juu ya maombi hayo utatolewa Oktoba 24 mwaka huu.