Wataalamu wa mipango nchini wameagizwa kutoa mapendekezo ya kiubunifu ambayo yataiwezesha nchi kunufaika na utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Agizo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakati akifungua kongamano la wanamipango kwa mwaka 2019 lililofanyika katika ukumbi wa wizara ya fedha na mipango jijini Dodoma.
Amesema agizo hilo linatokana na uwepo wa changamoto ya utekelezaji wa PPP nchini na kuwataka wataalamu hao kujadili ili kuona wapi nchi imekosea na kutoa suluhu ya namna ya kutatua changamoto hizo.
“PPP imefanikiwa sana ni kwenye sekta za kijamii najua tumefanya vizuri kwenye huduma za afya na elimu lakini kweye miradi ya miundombinu bado,” amebainisha Dkt. Mpango
Hata hivyo katika hatua nyingine amewagiza wataalamu hao kujadili namna bora ya kutanua wigo wa kukusanya kodi ili kuiwezesha nchi kujiendesha pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema kumekuwepo na shida katika suala la ukusanyaji wa mapato kwani hata idadi ya walipakodi inaonekana kuwa ni ndogo licha ya uwepo wa idadi kubwa ya wananchi nchini.
“Hakikisheni mnasimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuhakikisha yanatumika vyema ili kuweza kukuza uchumi wa nchi,” amebainisha Waziri Mpango.
Aidha amefafanua katika harakati za kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ni lazima nchi iweke mipango madhubuti ya kutafuta rasimali kutoka katika vyanzo mbadala vya mapato ya kuweza kugharamia miradi hiyo.
“Nchi inahitaji kuwa na uchumi wa kati sasa ni kuweka mipango madhubuti ya kutafuta rasimali kutoka katika vyanzo mbadala vya mapato,” ameongeza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake mchumi mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Lorah Madete amesema kupitia kongamano hilo washiriki watapata fursa ya kujadili mawasilisho yatakayoendana na dhima husika ikiwemo vyanzo vya ubunifu vya ugharamiaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa, sera, sheria na kanuni.
Kongamano hilo la siku mbili limekutanisha wataalamu wanaohusika na masuala ya mipango kutoka Wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, taasisi, sekretarieti za mikoa, mamlaka ya Serikali za mitaa na sekta binafsi.