Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, John Magufuli amesema kuwa Serikali imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kutokana na mlipuko wa Corona kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kwa kufanya hivyo.

Aidha, amesema madhara hayo yanaweza pia kuziathiri nchi 8 ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususan Bandari ya Dar es Salaam.

Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waumini wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mlimani, wilayani Chato mkoani Geita ambapo alihudhuria ibada ya Ijumaa Kuu jana.

Aidha amebainisha kuwa kutokana na madhara ya virusi vya Corona upo uwezekano mkubwa wa kutokea kwa upungufu wa chakula, hivyo amewataka Wananchi kuzalisha chakula cha kutosha.

Halikadharika amesisitiza wananchi waendelee kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari dhidi ya Corona kwa kufuata ushauri wa wataalamu na pia wasisahau kumuomba Mungu juu ya janga hili.

Mtihani mwingine A. Mashariki, Corona haijaisha Nzige wanarudi
Corona Tanzania: Vifo viwili vyaongezeka, wagonjwa wapya 7