Benki kuu ya Tanzania (BOT) imepitisha hatua mbalimbali za kisera ili kukabiliana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (covid-19).
Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 12 na Gavana wa BOT, Prof. Florens Luoga imeeleza hatua hizo kuwa ni pamoja na kushushwa kwa kiwango cha riba kwa mikopo inayokopwa na benki mbalimbali, kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5.
Punguzo hilo linaanza leo na hatua hiyo imefikiwa ili kuongeza wigo wa benki mbalimbali kukopa benki kuu kwa riba nafuu nahivyo kupunguza riba ya mikopo kwa wateja.
BOT imetoa agizo kwa mabenki na taasisi za fedha kutathmini kwa kina athari zinazotokana na mlipuko wa covid -19 kwenye urejeshaji wa mikopo, kujadiliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo itakayoonekana inafaa.
Imeahidi kutoa unafuu kwa mabenki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi bila upendeleo.
Hatua nyingine, benki kuu imeshusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa BOT kutoka asilimia 7 hadi asilimia 6 kuanzia tarehe 8 juni hatua inayotarajiwa kuongeza ukwasi katika sekta ya benki.
Hatua ya nne, Benki kuu imeongeza unafuu kwenye dahamana na hati fungani za serikali zinazotumika na benki kama dhamana wakati wa kukopa kutoka benki kuu.
Unafuu huo umepatikana kwa kupunguza kiwango cha dhamana kutoka asilimia 10 hadi asilimia 5 kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi 20 kwa hati fungani, hatua ambayo imeelezwa kuongeza uwezo wa benki kukopa kutoka benki kuu kwa unafuu zaidi kuliko ilivyokwa awali.
Imetoa agizo kwa makampuni yanayotoa huduma za fedha kwanjia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka sh. 3,000,000 hadi sh. 5,000,000 na kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka sh. 5,000,000 hadi 10,000,000 hatua ambayo imelenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali kufanya miamala mbalimali.
Hata hivyo BOT imeahidi kuendelea kufanya tathimini ya athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu covid -19 katika secta mbalimali za uchumi na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara ya athiri hizo.