Imeelezwa kuwa, kiungo Simba SC Said Ndemla ameongezewa mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kukipiga kwenye klabu hiyo kwenye msimu ujao baada ya kufikia muafaka mzuri na mabosi wake.
Awali, kiungo huyo alikuwa anatajwa kutimkia Young Africans ambayo ilikuwa inatajwa kuwania saini yake kwa ajili ya kuiimarisha safu ya kiungo ya timu hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa, mbali na makubaliano ya pande zote mbili na kusaini mkataba, pia sababu ya nidhamu ya mchezaji huyo inatajwa kuwa kichocheo kwa viongozi wa Simba SC kuvutiwa kuendelea kufanya naye kazi, licha ya kutokuwepo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachonolewa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kilichombakisha ni uwepo wa viungo wakabaji wachache katika timu hiyo, licha ya kuwepo mipango ya kushusha kiungo mkabaji mwingine wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa zaidi yake.
“Viongozi wamekubaliana kuwabakisha wachezaji wao waliowalea tangu wakiwa wadogo U20 kwa lengo la kutoondoka ndani ya kikosi hicho kutokana na uvumilivu waliokuwa nao wa kutoihama timu hiyo ambao ni Ndemla na Mkude (Jonas).
“Hivyo viongozi wamekubaliana kumbakisha, lakini amebakishwa kwa makubaliano ya kupambana katika timu ili apate nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.”
“Ndemla amekubaliana na hayo yote waliyokubaliana nayo huku akiomba mkataba wake uwe wa wazi utakaomruhusu kuondoka muda wowote kama akipata timu nje ya nchi,” alisema mtoa taarifa.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa hivi karibuni aliwahi kusema: “Kama uongozi tumepanga kuwabakisha wachezaji wote ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu kwa gharama yoyote lengo ni kuhakikisha tunasuka kikosi imara kitakachofanya vizuri katika msimu ujao.”