Miili ya wanafunzi 10 waliokufa kwa ajali ya moto uliounguza bweni la wavulana katika shule ya msingi Byamungu iliyopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera imeagwa leo na kukabidhiwa kwa wanafamilia tayari kwa mazishi.
Zoezi hilo limefanyika leo Septemba 18, 2020 katika viwanja vya shule hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt.Bashiru Ally Kakurwa ambaye amehudhuria kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
Akiongea katika hadhara hiyo Dkt. Bashiru amewapa pole wafiwa na jamii nzima iliyoguswa na msiba huo ambapo amewasihi wafiwa kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiitaka serikali pamoja na vyombo vya usalama kuendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.
Dkt.Bashiru ameitaka serikali na viongozi wa mkoa wa Kagera kusimamia maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli alipokuwa Bukoba na kuwataka wamiliki wa shule kuendelea kutoa ushirikiano pale watakapohitajika.
‘’Rais magufuli ameniagiza nije hapa kuwapa pole kwa msiba huu mkubwa lakini ameniagiza pia kuweka msisitizo wa maagizo yake aliyoyatoa ya kuhakikisha mazingira ya watoto wetu wanapokuwa shuleni yanakuwa salama,’’ amesema Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema kuwa serikali imekuwa bega kwa bega na wanakyerwa na hasa wafiwa kwa kuhakikisha marehemu wanahifadhiwa vizuri pamoja na majeruhi kutibiwa ambapo amesema kuwa tayari zimeundwa kamati za uchunguzi kwenye shule zote za bweni mkoani humo kwa ajili ya kuangalia miundombinu.
Ajali hiyo ya bweni kuungua moto ilitokea usiku wa kuamkia Septemba 14 mwaka huu katika shule ya msingi Byamungu Islamic na kusababisha vifo vya watoto 10 na wengine saba kujeruhiwa.