Waziri mkuu mteule wa Lebanon Mustapha Adib amejivua jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri baada ya karibu mwezi mmoja wa juhudi za kupanga baraza la mawaziri lisiloegemea upande mmoja.
Adib amesema kuwa anaachana na jukumu la kuunda serikali, kufuatia mkutano na Rais Michel Aoun, baada ya juhudi zake kukumbwa na matatizo haswa kutokana uteuzi wa waziri wa fedha.
Wakati huo huo, spika wa bunge la nchi hiyo Nabih Berri, ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la Amal la madhehebu ya kiislamu ya Kishia, amesema kuwa kundi lake litaendelea kudumisha mpango wa Ufaransa.
Lebanon iko katika hali ngumu ya kiuchumi kutokana na mlipuko mkubwa uliotokea Agosti 04, jijini Beirut ambapo watu takriban 200 walifariki na wengine zaidi ya 5000 kujeruhiwa.
Serikali ya Lebanon iliyopita ilijiuzulu kutokana na shinikizo la machafuko baada ya mlipuko, ulioathiri sehemu kubwa ya mji mkuu Beirut, mlipuko ambao kwa mujibu wa Benki ya Dunia unakadiriwa kusababisha hasara ya dola bilioni 4.6 kutokana na uharibifu wa majengo na miundombinu uliotokea.