Kocha Msaidizi wa Young Africans, Juma Mwambusi, amefichua siri ya kuanzishwa kwa kiungo kutoka nchini Angola Carlinhos kwenye mchezo wa jana Jumapili, Septemba 27 dhidi ya Mtibwa Sugar, uliomalizia kwa wababe wa Jangwani kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.
Kwa mara ya kwanza kiungo huyo aliesajiliwa mwezi uliopita na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wanachama, alianzishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans, tangu kuanza kwa msimu huu 2020/21, Septemba 06.
Mwambusi amesema kuanzishwa kwa kiungo huyo ulikua mpango maalum wa benchi la ufundi, kwa kuamini alikua na kila sababu ya kucheza kutokana na kuonyesha utofauti mkubwa wakati wakijiandaa kuikabili Mtibwa Sugar.
“Unajua watu wengi wamekariri Carlinhos sio mzuri sana kwenye viwanja kama hivi, lakini tulikuja na mpango wa kumuanzisha kwenye mchezo tofauti na michezo iliyopita kwa sababu anaweza kutoa kitu cha tofauti cha kuinufaisha timu na ndicho alichokifanya,” Amesema Mwambusi.
Carlinhos anaendelea kujizolea sifa ndani ya kikosi cha Young Africans kwa kucheza vizuri mipira iliyokufa, kwani alichangia kupatikana kwa bao pekee la klabu hiyo, na hiyo ni mara yake ya pili baada ya kufanya hivyo dhidi ya Mbeya City, pale alipopiga kona na Moro kufunga kwa kichwa.
Jana mchezaji huyo raia wa Angola alipiga tena kona na kumkuta Moro aliyefunga dakika ya 61 na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na pointi tatu na kufikisha jumla ya alama 10 baada ya mechi nne sawa na Simba iliyo nafasi ya pili, lakini Young Africans ikishika nafasi ya tatu kutokana na tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Ushindi huo unavunja mwiko baada ya Young Africans kushindwa kuibuka na ushindi katika uwanja huo kwa misimu mitatu mfululizo, ambapo imefungwa mara mbili na kutoka sare mara moja, pia ni sawa na kuizidi mbinu Simba, kwani walitoka sare ya bao moja kwa moja na Mtibwa kwenye uwanja huo huo hivi karibuni katika mchezo wa ligi hiyo.