Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kuwa Awamu ya Pili ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2020/2021 itaanza rasmi Jumatatu tarehe 12 hadi 18 Oktoba, 2020.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa awamu ya kwanza ya udahili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 imekamilika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo jumla ya waombaji 90,572 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 74 vilivyoidhinishwa kudahili katika awamu hii ya Kwanza ya udahili kwa mwaka wa masomo 2020/2021.
Kwa upande wa nafasi, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 157,770 ikilinganishwa na nafasi 149,809 mwaka uliopita, hili likiwa ni ongezeko la nafasi 7,961 za Shahada ya Kwanza sawa na asilimia 5.3.
Katika Awamu hii ya Kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 60,621 sawa na
asilimia 69.9 ya waombaji walioomba udahili wameshapata udahili vyuoni.
TCU inawataka waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo tarehe 09 hadi 17 Oktoba, 2020 kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.
Majina ya waliodahiliwa katika awamu hii yanatangazwa
na vyuo husika.