Mwadui FC wametuma salamu kwa vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC, kuelekea pambano la mzunguuko wasita litakalowakutanisha keshokutwa Al-Khamis, Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.

Mwadui FC wamekua wakifanya mazoezi jijini humo tangu kusimama kwa Ligi Kuu, kwa ajili ya kupisha mchezo wa kimataifa wa kirafik kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Burundi (Intamba Murugamba), uliomalizika kwa Stars kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

Wakiwa jijini Dar es salaam, Mwadui FC walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Young Africans mwishoni mwa juma lililopita, Uwanja wa Azam Complex Chamazi, na kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

Mkuu wa benchi la ufundi la Mwadui FC, Khalid Adam amesema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo dhidi ya Azam FC, na ana uhakika watapambana ili kupata matokeo chanya.

“Wachezaji wapo vizuri na maandalizi yapo sawa matumaini yetu ni kuona kwamba tunapata matokeo mazuri ambayo yatatufanya tuzidi kuwa kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo.”

“Ligi ina ushindani mkubwa kwa sasa hilo lipo wazi na kila mmoja anajua hivyo nasi ni lazima tufanye vizuri kupata matokeo.

“Tunakutana na timu bora hilo hakuna ambaye hajui ila nasi pia tupo vizuri, kuanza vibaya haina maana kwamba wachezaji hawana uwezo wa kupata matokeo,” amesema Kocha Khalid.

Kabla ya kusimama kwa Ligi Kuu, Mwadui FC waliifunga Namungo FC bao moja kwa sifuri katika mchezo wa mzunguuko watano, uliochezwa Majaliwa Stadium, mkoani Lindi.

Lipumba kuboresha mfumo wa fedha
Trump apona Corona