Kamati ya Maadili ya TFF imeshindwa kutoa uamuzi juu ya shitaka la kimaadili linalomuhusu kiungo wa Simba, Bernard Morrison, kwa sababu mchezaji huyo kutoa udhuru na kushindwa kufika kwenye kamati hiyo kwa madai ya kukabiliwa na majukumu ya klabu yake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Wakili Kichere Mwita Waissaka amesema Morrison alituma wawakilishi ambao ni mawakili wake, lakini kutokana na uzito wa shauri lenyewe, kamati inamuhitaji mlalamikiwa mwenyewe badala ya wawakilishi ambao wasingeweza kujibu baadhi ya maswali.

“Kamati iliona kwamba kuna maswala yanatakiwa kujibiwa nay eye mwenyewe badala ya wawakilishi, kwahiyo suala lake liliahirishwa,” amesema Kichere.

Morrison anakabiliwa na shtaka la kudharau kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kwa kitendo chake cha kusaini mkataba na Simba wakati shauri lake dhidi ya Yanga kuhusu mkataba wake likiwa bado halijaamuliwa.

Kuhusu rufaa ya Yanga kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS), Kichere amesema rufaa hiyo haihusiani na shauri lililopelekewa kwenye kamati hiyo, kwani rufaa ya Yanga inahusu usajili wakati shauri lililo mbele yao linahusu maadili.

WB, IMF wawaomba G20 kuzisamehe madeni nchi masikini
Kenya: Wanafunzi wenye mimba waruhusiwa kurudi Shule