Kiungo na mshambuliaji wa pembeni kutoka Ivory Coast Nicolas Pepe, wameomba radhi mashabiki, wachezaji na meneja wa klabu ya Arsenal kupitia kurasa zake za mtandao wa kijamii, kufuatia adhabu ya kadi nyekundu ailioneshwa wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Leeds United, juzi Jumapili (Novemba 22).
Licha ya kucheza pungufu kwenye mchezo huo Arsenal, walipambana na kulazimisha matokeo ya sare ya bila kufungana, huku Leeds United wakiwa nyumbani.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Ezgjan Alioski mapema kipindi cha pili, hivyo atakosa michezo mitatu ya Ligi Kuu ya England.
Pepe amefanya maamuzi ya kuwaomba radhi mashabiki wa Arsenal, huku akionyesha kujutia kitendo cha utovu wa nidhamu alichokifanya.
“Nimeiangusha timu yangu katika wakati muhimu wa mchezo dhidi ya Leeds United, sina visingizio kwa tabia yangu. Samahani sana na ningependa kuomba radhi kwa mashabiki, wachezaji wenzangu, meneja wangu na kila mtu ndani ya klabu.”
Pepe amekuwa na wakati mgumu kupata namba ya kuanza chini ya meneja Mikel Arteta kwenye Ligi ya England, licha ya kuchaguliwa baada ya Reiss Nelson kenye mchezo dhidi ya Leeds.
Hata hivyo changamoto ya kuongezeka kwa majeruhi ndani ya Arsenal, Pepe anaweza kupewa nafasi ya kujirekebisha, keshokutwa Alhamisi wakati Gunners watakapocheza ugenini dhidi ya FK Molde ya Norway kwenye mchezo wa Europa League.