Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha amesema Serikali imepiga marufuku uuzaji, usafirishaji na ulaji wa nyama ya nguruwe (kitimoto) kwa muda usiojulikana wilayani humo baada ya kujitokeza kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe ambao umesababisha vifo vya nguruwe zaidi ya 500.
Macha ametoa agizo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Akitoa taarifa ya kuingia kwa ugonjwa wa homa kali ya nguruwe ( African Swine Fever), wilayani humo mwezi uliopita
“Tumelazimika kuchukua hatua hiii ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo ambao unaua nguruwe kwa kasi, watakaobainika kukiuka agizo hili watachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema Macha.
“Kwa sasa Kahama biashara ya nguruwe imepigwa marufuku, lengo letu ni kudhibiti ugonjwa huu, wataalamu wetu wanaendelea kufanya utafiti ili kuhakikisha wanaudhibiti mapema ili kuzuia madhara yasijitokeze zaidi” ameongeza Macha.
Macha amewataka walaji wa nyama ya nguruwe (kitimoto) kuacha kula nyama hiyo, hadi watakapotangaziwa na serikali, na kuwashauri kula nyama nyingine kama za ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ambao ugonjwa huo haujawaathiri.