Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara *TPLB* imethibitisha kuendelea kwa mshike mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, ambao upo kwenye mzunguuko wake wa pili.
Ligi Kuu Tanzania Bara ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya taifa ya Tanzania *Taifa Stars*, sanjari na maombolezo ya aliyekua Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli, aliyefariki duniani Machi 17 na kuzikwa Machi 26 nyumbani kwake Wilayani Chato mkoani Geita.
TPLB wamethibitisha kuendelea kwa Ligi hiyo baada ya kumalizika kwa siku 21 za Maombolezo ya kiongozi huyo, ambaye ataendelea kukumbukwa na watanzania wote kwa uthubutu na utendaji kazi uliotukuka wakati wa uhai wake.
Katika ratiba hiyo vinara wa Ligi Kuu Young Africans wenye alama 50 watakuwa wenyeji wa KMC FC Aprili 10 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Azam FC wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo kwa kumiliki alama 41 watapepetana na Mtibwa Sugar Aprili 09.
Mabingwa watetezi Simba SC wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 46 walipaswa kucheza dhidi ya Ruvu Shooting April 10, lakini kutokana na majukumu yao kimataifa mchezo huo umeahirishwa.
Simba SC watarejea tena dimbani kuendelea na mshike mshike wa Ligi Kuu Aprili 14 kwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.