Uongozi wa klabu ya KMC FC umetoa mapumziko mafupi kwa wachezaji wake kuanzia Mei 17 na kwamba watapaswa kurejea kambini Mei 25 ili kuendelea na maandalizi ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Dododma Jiji.

Mapumziko hayo yametokana na Timu ya KMC FC kutokuwa na mchezo wowote wa mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja ambapo kwa mujibu wa ratiba ya Bodi ya Ligi ni kwamba KMC FC itaendelea na mchezo wa Ligi Kuu kuanzia Juni 17 mwaka huu katika Uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma dhidi ya Dodoma Jiji.

Aidha kufuatia mapumziko hayo, Kocha Mkuu John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habibu Kondo wataweka utaratibu wa kufanya mazoezi pindi wachezaji watakaporejea kambini sambamba na kucheza mechi nyingi za kirafiki kwa lengo la kuendelea kujiimarisha na hivyo kufanya vizuri kwenye michezo iliyobakia.

“Tumetoka kupoteza mchezo muhimu dhidi ya Azam FC , lakini bado haitukatishi tamaa kuendelea kupambania nafasi ya Nne, hivyo mapumziko haya ni maalumu kwa wachezaji wetu, na kwamba tukirudi kama Timu uongozi kwa ujumla tutaendelea kuweka nguvu zaidi kwenye michezo yetu iliyobaki na hivyo kufanya vizuri ili mwisho wa siku tufikie malengo ambayo tumejiwekea.

Hata hivyo KMC FC hadi sasa imecheza michezo 29 na kufikisha alama 41 na kuendelea kusalia katika nafasi ya tano huku ikiwa imebakiza michezo mitano kabla ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu soka Tanzania bara 2020/2021, ambayo ni dhidi ya Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, JKT Tanzana , Simba pamoja na Ihefu.

Imetolewa leo Mei 18

Na Christina Mwagala

Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC

Badru kuiongoza Mtibwa Sugar leo
Young Africans yavamia Dodoma