Mashabiki wa Yanga wakisikia kuna taarifa za kurejea kwa aliyekuwa nahodha wao wa zamani, Ibrahim Ajibu wanageuka mbogo hawataki kusikia hilo na sasa uongozi wao umeweka bayana msimamo wa hatma ya mshambuliaji huyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinus amefunguka kuwa katika mkoba wake ana majina kadhaa ya wachezaji wapya wa maana wanaotakiwa kusajiliwa msimu ujao lakini hakuna jina la Ajibu wala mchezaji yeyote kutoka Simba.
“Hatuwezi kumsajili Ajibu kwa historia yake makosa ya namna hiyo hayawezi kufanyika sasa, hajacheza karibu msimu mzima huu, mchezaji wa ndani tutakayemsajili kila mtu atakubali takwimu zake kwa kile ambacho amekifanya ndani ya msimu mmoja unaoisha au zaidi.
“Tutasajili wachezaji Bora msimu ujao, ni kazi ambayo tulianza muda mrefu, tunafahamu usajili wakati mwingine ni kama kamari lakini safari hii tutakuwa makini zaidi tunajua shida ya kikosi chetu.
Ameongeza katika usajili wao ujao, wanafanya kazi kwa kumshirikisha kocha wao, Nasreddine Nabi kuangalia ubora wa wachezaji
“Tunaheshimu uwezo wa Ajibu lakini ni vigumu kutetea usajili wake kwa mtu ambaye kocha hajamuona akicheza , msimu mzima amekuwa akisotea benchi.”