Kocha Mkuu wa Klabu ya Young Africans, Mohammed Nasreddine Nabi, amesema Mlinda Mlango Metacha alifanya makosa kwa kushindwa kuonesha kiwango cha kuukabili mpira uliozaa bao la pili la Ruvu Shooting, kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana Alhamis, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Nabi ameweka wazi suala hilo, kufuatia lawama kuendelea kuelekezwa kwa mlinda mlango huyo, ambaye alizua vurugu kwa baadhi ya mashabiki waliooneshwa kuchukizwa na kile alichokifanya akiwa katika majukumu yake, katika mchezo huo uliomalizika kwa Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa mawili.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema mchezaji huwa anaharibu na anapoharibu mashabiki wanapaswa kuendelea kuwa wamoja na wachezaji, na haitakiwi mchezaji akikosea watu wamuhukumu.
“Mlinda Mlango ni mchezaji ambaye akifanya kosa huwa linaonekana palepale, na ni kweli Metacha amefanya kosa lakini kilichomfanya akasirike ni mashabiki kumshambulia badala ya kumfariji.” Amesema Kocha Nabi.
Hata hivyo Kocha Nabi akamkingia kifua Metacha Mnata kwa kusema asichukuliwe kama mtovu wa nidhamu ama mkosa adabu, bali alichokiona kwa Mlinda Mlango huyo ni hasira za kuchukizwa na kilichokua kikisemwa dhidi yake
“Wachezaji wangu sio kwamba hawana adabu, na wao ni binadamu pia, kama ingekuwa wewe umeenda mtaani kwako halafu majirani wakupigie makelele na kukutolea maneno mabaya, huwezi kubaki kichwa chini, kitu alichofanya Metacha ni kutokana na kushambuliwa na mashabiki wake.” Amesema.
Tayari Uongozi wa Young Africans umetangaza kumsimamisha kwa muda Metacha Mnata kwa kosa la utovu wa nidhamu aliouonesha jana baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.
Metacha alifikia hatua ya kuonesha utovu wa nidhamu baada ya kuchukizwa na maneno makali yaliyotolewa dhidi yake na baadhi ya mashabiki wa Young Africans, ambao walidai alifungisha kwa makusudi bao la pili kwenye mchezo huo.
Ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Ruvu Shooting, unaiwezesha Young Africans kufikisha alama 64, ambazo zinaendelea kuiweka nafasi ya pili klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.