Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkozni Morogoro, Mathayo Masele, amewakumbusha maafisa ugani kuzingatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa wakati akizindua Kampeni ya Kilimo cha alizeti mkoani Singida hivi karibuni la kumtaka kila afisa kilimo kuwa na shamba la mfano.
Rc Masele, ameyasema hayo katika uzinduzi kituo cha usambazaji wa teknolojia za kisasa za kilimo kupitia taasisi ya utafiti wa kilimo nchini TARI, kilichopo viwanja vya J.K Nyerere Nanenane mkoani Morogoro ambacho kimesheheni wataalamu watakaotoa mafunzo kwa wakulima na huduma za kiugani kwa kipindi chote cha mwaka.
Naye , Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo amesema kuwa shabaha kubwa ya kituo hicho ni kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa wakulima.
“TARI tumejipanga vizuri katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa kuhakikisha mkulima analima kisasa kwa kuzingatia kanuni zote za kilimo bora, ndio maana kituo hiki kina wataalamu mbalimbali wa kilimo wakiwemo watafiti,” Amesema Mkamilo.
Kituo hicho kilichopo viwanja vya J.K Nyerere Nanenane mkoani Morogoro sasa kinakuwa cha pili kikitanguliwa na kituo kama hicho kilichozinduliwa mapema mwaka jana, eneo la Nyakabindi, Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.