Polisi nchini Kenya wanamshikilia kijana mwenye umri wa miaka 22 aliyekamatwa akichukua damu kwenye mwili wa marehemu alipotembelea chumba cha kuhifadhia miili (mortuary) katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mtuhumiwa huyo alikutwa akichukua damu kwa siri kutoka kwenye mwili wa Clinis Atieno Ojenge (40), aliyeuawa kwa kupigwa risasi.
Marehemu alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Gul Kagembe, Kaunti ya Rangwe. Alipigwa risasi Jumanne usiku wiki iliyopita.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alifika katika chumba hicho akitokea eneo la Ndhiwa, alifuata taratibu zote za kupata kibali cha kuingia kuona mwili wa mpendwa wake. Alitaja jina na akaruhusiwa na kwamba aliingia akiwa na dereva bodaboda aliyeongozana naye.
Kwa mujibu wa wahudumu wa chumba hicho cha kuhifadhia miili ya marehemu, waliporuhusiwa walienda moja kwa moja na kuangalia mwili wa marehemu waliyemtaja. Lakini wakati wanatoka ndipo walipofanya jambo lisilo la kawaida.
“Wakati wanaanza kutoka nje ya chumba, aliona mwili wa mwalimu, badala ya kuendelea kutoka nje aliinama karibu na mwili na kuanza kuchukua damu zilizokuwa zinatoka kwenye pua ya marehemu,” mhudumu wa chumba hicho anakaririwa.
Ameeleza kuwa baada ya kuona kitendo hicho, wahudumu waliwaita walinzi waliokuwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Kaunti hiyo na wakafanikiwa kumkamata.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kaunti ya Homa Bay, Bi. Monica Berege amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Amesema wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano kufahamu sababu za kutaka kuchukua damu ya marehemu.
Bi. Berege amesema wameanzisha pia uchunguzi ili kubaini kama kuna uhusiano wa tukio hilo na mauaji ya mwalimu.