Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa (TCM) limeanza Mkutano wao wa 17 unaotarajiwa kufanyika kwa siku tano jiji Dar es Salaam
Mkutano huo utakaofanyika kuanzia Juni 21 hadi 25 Juni 2021 unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa programu na miradi, maamuzi na maagizo ya mikutano ya awali katika sekta za miundombinu ya uchukuzi mawasiliano na hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo unatarajiwa kupitisha Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Usalama Barabarani (EAC Road Safety Strategy), ambao unaambatana na Mpango Kazi wa Usalama Barabarani wa kipindi cha miaka 10 (2021-2030,) ukilenga kuchukua hatua madhubuti za kuboresha usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti athari zinazopelekea ulemavu, upotevu wa maisha pamoja na mali kutokana ajari za barabarani.
Aidha, unatarajiwa kuridhia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Uendeshaji na Usimamizi wa Anga la Juu la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za anga, kuimarisha usalama na mawasiliano ya usafiri wa anga kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia unatarajiwa kuridhia uanzishwaji wa Taasisi ya Mawasiliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutakoambatana na kupitisha Andiko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sambamba na hayo, Mawaziri hao wanatarajiwa kukubali kuibadili Taasisi ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki (East African Communication Organization –EACO) kuwa Taasisi rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia sekta ya Mawasiliano ndani ya Jumuiya.
Kama ilivyo ada kwa Mikutano ya Baraza la Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika katika ngazi tatu, Mkutano huu pia utafanyika katika ngazi tatu ambazo ni, Ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 22 Juni, 2021; Makatibu Wakuu, tarehe 23 na 24 Juni, 2021 na Mawaziri, tarehe 25 Juni, 2021.