Baada ya kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Namungo FC jana Jumatatu (Juni 21), Benchi la Ufundi la Azam FC limetoa sababu ya kushindwa kuwika kwenye uwanja wa ugenini huko mkoani Lindi.
Azam FC inyoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ilikua inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo dhidi ya Namungo FC, kutokana na mwenendo wake kabla ya mchezo huo, lakini mambo yaliwaendelea kombo baada ya dakika 90.
Kocha Msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati amesema, kikosi chao kilipambana kusaka alama tatu muhimu na kilionesha lengo hilo ndani ya dakika 90, lakini mipango ya wapinzani wao iliwazuia kufikia lengo.
Amesema licha ya matokeo hayo, bado wanashukuru kupata alama moja kwenye mchezo huo wa ugenini, ambao amekiri ulikua mgumu.
“Namungo ni timu nzuri na kila timu kwenye mchezo ilikuwa inahitaji ushindi na mwisho wa siku hakuna ambaye ameshinda.”
“Mbinu ya Namungo ilikuwa ni sawa na kwetu na kwa kuwa tumepata pointi moja kwetu ni nzuri na ilikuwa ili ushinde ilikuwa unahitaji kushinda kwa kutumia mipira ya kutengwa.”
“Bahati mbaya sana kwetu Namungo waligundua hilo na mwisho wa siku hatukuweza kupata faulo hizo na tukaambulia pointi moja,” amesema Kocha Bahati.
Kwa matokeo hayo Azam FC imefikisha alama 64 huku ikicheza mchezo 32, na upande wa Namungo FC inayoshika nafasi ya tano imefikisha alama 43.