Kaimu Mkurugenzi wa Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Lazaro Mwambole amesema shirika hilo litaendelea kutilia mkazo kusimamia maswala ya viwango na udhibiti ubora wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mifuko.
Ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo kwa wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya Non-Woven na mifuko mingine ya plastiki iliyofanyika makao makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.
“TBS imekuwa ikihakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo mifuko ya Non-Woven bags, mifuko ya plastiki iliyoruhusiwa zinakidhi matakwa ya viwango kwa mantiki hiyo TBS itaendelea kuhakikisha kwamba biashara zinafanywa katika mifumo inayoeleweka na kukubalika kisheria sambamba na kanuni zinazosimamia mifumo ya viwango na udhibiti ubora”. Amesema Mwambole.
Aidha Mwambole amesema ikiwa watumiaji hawawezi kupata bidhaa yenye ubora na inayoendana na mahitaji yake, husababisha kuwepo kwa kwa malalamiko juu ya thamani ya maisha yao na fedha zao.