Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Merrisone Mwakyoma amesema IGP Siro atafanya ziara katika mkoa huo Julai 3, 2021 na kuzunguma na wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha ulinzi shirikishi.
Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi Kamanda Mwakyoma ametaja makundi ambayo IGP Sirro atazungumza nayo ambayo ni viongozi wa dini, wazee, wenyeviti wa vijiji, maofisa watendaji wa vijiji na wote wanaoshirikiana na polisi kufanikisha ulinzi shirikishi.
Amesema polisi hawawezi kumaliza uhalifu wenyewe bila kushirikiana na jamii kwa kuwa wahalifu wapo mitaani na wanaishi nao.
“Mara nyingi ushirikiano wa jamii unafanikisha kazi ya polisi na tunapowaelewesha watueleze nasi tunatunza siri kwa watoa taarifa na kuendelea kushirikiana,” amesema Mwakyoma.
Amesema ndio sababu Sirro anakutana na makundi hayo ili wananchi waendelee kushirikiana na polisi kutokomeza uhalifu kupitia ulinzi shirikishi.
“Wakati mwingine jamii hulaumu polisi kuwa uhalifu umezidi wakati mwananchi huyo hawajibiki kutoa taarifa pindi anapobaini viashiria vya uhalifu katika eneo lake,” amesema Mwakyoma.