Shabiki wa klabu ya Young Africans Hussein Mangsul ameutaka Uongozi wa klabu hiyo kutimiza ahadi ya kumkatia tiketi, ili aweze kuuwahi mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC ambao utaunguruma keshokutwa Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Shabiki huyo mkazi wa Kigoma ambaye alichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari baada ya kutembea kwa miguu hadi Dar kwa ajili ya kuangalia mchezo wa watani wa jadi uliokua umepangwa kuchezwa Mei 08, amesema aliahidiwa na uongozi wa klabu hiyo watamtumia tiketi ya ndege kwenda kuutazama mchezo wa Julai 03.

Akizungumza na kituo cha CG FM cha mkoani Tabora, Mangsul amesema: Nasubiri tiketi nilioahidiwa na Uongozi wa Young Africans, ili niweze kwenda Dar es salaam kushuhudia mchezo wa keshokutwa Jumamosi.”

“Nina imani uwepo wangu kwenye mchezo huo utaniwezesha kutimiza lengo niliolokua nayo mwezo Mei, baada ya kutembea kwa miguu kutoka hapa Kigoma hadi Dar es salaam, lakini bahati mbaya mchezo uliahirishwa.”

Hata hivyo Mangsul ambaye alirejeshwa mkoani Kigoma usafiri wa ndege amedai iwapo Uongozi wa Young Africans hawatatimiza ahadi ya kumtumia tiketi ya ndege kwenda kutazama mchezo huo watafungwa na wasimlaumu mtu kwa kile kitakachowapata. Shabiki huyo amesema dawa ya kuifunga Simba anayo yeye na sio mtu mwingine.

“Kama hawatatimiza ahadi yao tusilaumieane, kuna umuhimu mkubwa sana mimi kuwepo Dar es salaam kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Simba SC, ninaijua dawa ya hawa jamaa ili wasitufunge, sasa kazi ipo kwa walioniahidi.” amesema Shabiki Mangsul.

Simba SC inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 73, Jumamosi (Julai 03) itakuwa mwenyeji wa Young Africans iliyo nafasi ya pili kwa kumiliki alama 67, huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 63.

Pigo benchi la ufundi Simba SC
IGP Sirro kufanya ziara Mkoa wa Manyara