Saa chache kabla ya kuwavaa Maafande wa Jeshi la Polisi (Polisi Tanzania FC) katika uwanja wa Ushirika mkoani Kilimanjaro, KMC FC wamechimba mkwara, kwa kusisitiza wanazihitaji alama tatu za mchezo huo wa kwanza kwa msimu wa 2021/22.
KMC FC yenye maskani yake jijini Dar es salaam, tayari imeshawasili mkoani Kilimanjaro kwa mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka nchini baada ya kushuhudia vikosi vya timu zote vikiwa na sura mpya za wachezaji waliosajiliwa kwa msimu huu.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya KMC FC Christina Mwagala amesema kikosi chao kimejiandaa vizuri kuelekea kwenye mchezo huo, ambao utapigwa majira ya saa nane mchana, huku akisistiza wanaiheshimu Polisi Tanzania FC.
Amesema wanatambua Ligi Kuu msimu huu ina changamoto kubwa ya ushindani, lakini KMC FC imejipanga vizuri ili kufikia malengo ya kufanya vizuri, hivyo wataanza na Polisi Tanzania FC.
“Kuanza kwa ligi kwetu sisi ni maandalizi na mwanzo mzuri ni jambo ambalo tunalihitaji hivyo tutaanza kufanya mbele ya Polisi Tanzania, maandalizi ambayo tumeyafanya ni makubwa na tunaamini tutafanya vizuri.
“Kikubwa mashabiki wazidi kuwa nasi, hatutawaangusha na tutaendelea na pira letu lile, pira spana na pira kodi na kwa usajili ambao tumefanya ni moto wa kuotea mbali,” amesema.
Nyota ambao ni wapya ndani ya kikosi cha KMC FC ni na Faroukh Shikalo ambaye alikuwa anakipiga Young Africans pamoja na Miraj Athuman aliyekuwa anawatumikia Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.