Kalamu ya @swalehmawele
Ghafla tu nimemkumbuka mundu yule, ni huyo mwana wa Sengerema anaevitawala vinywa vya wadau wa soka katika ardhi ya mama Samia na kuwa mada kuu katika vijiwe vya kahawa.
Si katika vibanda umiza pekee bali hata kwa wale walevi wa masumbwi wanalitaja jina lake mara nyingi, aliwahi kunishibisha usemi mmoja kati ya maswahiba zangu wa karibu, wanapokukopesha imani ni jukumu lako kuwalipa uwezo.
Ni ngumu kuzirudisha nyakati zilizofaulu kutuacha bali kumbukumbu za matendo yake zitaendelea kujivinjali katika kila iitwayo leo, nazikumbuka dhihaka na kebehi za wengi waliochagua kutomuamini.
Ni yeye tu aliechukuliwa katika uzito wa sufi na thamani yake kufananishwa na unyoya, muda ndie hakimu wa kweli na kinachotokea sasa kinaishi katika yale waliyoyanena waliotutangulia katika uso wa Dunia.
Hatuijui kesho yetu, maisha yetu yamegubikwa na fumbo zito na mitihani ya Kidunia inayojidhihirisha katika kila uchao, si kwa jeuri yetu na vile tunavyoviendea mbio, si kwa ufedhuri wa ndimi zetu utakaotutakasa matongotongo.
Ni imani tu ya Sven Vandenbroeck ikawa ni msingi wa kila kitu na kesho yake kujisogeza kwa nuru, ni kama alishaweka alama katika moyo wa Didier Gomes Da Rossa nyuma ya Pascal Wawa na Joash mwana wa Onyango.
Ni Kennedy Wilson wa Juma, unataka nini kengine kwa mlinzi huyu mahiri, si tajiri wa usemi kinywani mwake bali miguu tu inapozipiga kelele na kuzinyanyasa ngoma zetu za sikio.
Haikuwahi kuwa shida alipoumia Onyango wala hayakudhihiri manung’uniko alipokosekana Pascal Wawa, ni Kennedy tu alieizuia kila hatari iliyosimama ndani ya uwezo wake na Simba kubaki salama kwa wapinzani wake wa karibu.
Asante Kennedy Juma, asante kwa Jasho lako ndani ya kiwanja na hakika unawalipa uwezo wale wachache waliochagua kukuamini katika siku zilizofaulu kutuacha, Ubarikiwe sana mlinzi mwengine hodari.