Kocha Msaidizi wa Namungo FC, Godfrey Okoko wamesema mchezo wa leo Jumatano (Novemba 03) dhidi ya Simba SC, wanaupa umuhimu mkubwa, kufuatia hitaji lao la kusaka alama tatu muhimu.
Namungo FC watakutana na Simba SC kuanzia saa moja usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku historia ikiwahukumu, kwani hawajawahi kuifunga klabu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam.
Kocha Okoko amesema kikosi chao kitaingia uwanjani kwa kushambulia kwa sababu wanazihitaji mno alama tatu, kutoka kwa Simba SC.
“Kama Simba SC ambavyo wanazitaka na sisi pia tunazitaka, wachezaji wetu wako vizuri, hatuna majeruhi wala kadi nyekundu. Tunachotaka wachezaji wetu waingie, wapambane na kufanya kile ambacho tumewaagiza,” amesema kocha huyo raia wa Burundi.
Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Kwa upande wa Namungo FC, mara ya mwisho kushuka dimbani ilikua dhidi ya Azam FC, ambapo walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Kufuatia hali hiyo, timu zote mbili zinahitaji ushindi katika mchezo wa leo, hali ambayo inadhihirisha mpambano utakua mkali na wa kuvutia.
Simba SC yenye alama 8 baada ya kushuka dimbani mara nne, inashika nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Namungo FC yenye alama 5 baada ya kushuka dimbani 4, ipo nafasi ya 11.