Kaimu Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Thierry Hitimana, amesema anaamini kikosi chake kitafanya vizuri kwenye mchezo wa leo Jumatano (Novemba 04) dhidi ya Namungo FC, kwa sababu hata mchezo uliopita, walitengeneza nafasi nyingi, lakini kwa bahati mbaya tu walishidwa kuzitumia.

Hitimana ambaye akemabidhiwa jukumu la kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu klabuni hapo, baada ya kuondoka kwa Kocha Didier Gomes, amesema amekiandaa vyema kikosi chake, na ana aamini kila mchezaji anajua umuhimu wa ushindi dhidi ya Namungo FC.

Amesema katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, kikosi chake kilipambana na kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini haikuwa bahati kwao ya kuibuka na ushindi ambao ungewapa alama tatu, ila leo Jumatano anaamini mambo yatakwenda vizuri kufuatia maboresho aliyoyafanya mazoezini.

“Tumejiandaa vizuri, tunakumbuka kuwa mchezo uliopita tulitoka sare nyumbani, tukakosa pointi tatu, watu hawakufurahia, inavyoonekana haikuwa siku yetu, unajua siku zote haziko sawa na hiki ni kama kipindi cha mpito baada ya miaka minne ya mafanikio, kitapita tu.”

“Kama uliona kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko, timu ilianza kucheza na kushambulia, bahati mbaya tu, mabao yalikataa kuingia, lakini kwenye mchezo hii hali inaweza kuwa tofauti,” amesema kocha huyo ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Namungo FC.

Naye Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola, amekiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu hakuna mchezo wowote ambao hucheza na timu hiyo ukawa rahisi.

“Hakuna mchezo wowote ambao tunacheza na Namungo ukawa rahisi, lakini tumejiandaa kupata ushindi, tumejipanga kupata matokeo mazuri.”
“Ni kweli tuna tatizo la kufunga mabao na hiyo inatokana na presha waliyonayo wachezaji wetu kwa sasa na muda ni mdogo wa kulishugulikia, ila tunapambana nalo,” amesema Matola

katika hatua nyingine Kocha Hitimana amethibitisha kuwa atawakosa Mugalu na Sakho ambao bado hawajawa fiti, huku wakizalisha majeruhi wengine kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, Mzamiru na Kanoute.

Namungo FC yatuma salamu Simba SC
Khalid Aucho aikana Simba SC