Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison amefunguka kwa mara ya kwanza, baada ya kikosi cha Simba SC kuwa na mwanzo mbaya katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Morrison amefunguka hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, ambapo amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuendelea kuwa na imani na timu yao.
Kiungo huyo ameandika: “Mpira unaweza kuwa wa kikatili na wakati mwingine kuwa mzuri. Michezo iliyopita imetuletea huzuni kwetu na kuwapa furaha wapinzani wetu. Na hivyo ndio mpira ulivyo”
“Matokeo yaliyopita yametupotezea hali ya kujiamini, na kupoteza upendo tuliokuwa tunaupata kutoka kwa mashabiki”
“Ni hatua fulani katika mpira, naombeni tuwe pamoja tena naimani mambo yatakuwa vizuri “
WE ARE WHO WE ARE BECAUSE OF YOU SO DON’T LEAVE US❤️
Benard Morrison (@bm3gh )
Leo Jumatano (Novemba 03) Simba SC inakwenda kucheza dhidi ya Namungo FC, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Kwa upande wa Namungo FC, mara ya mwisho kushuka dimbani ilikua dhidi ya Azam FC, ambapo walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Kufuatia hali hiyo, timu zote mbili zinahitaji ushindi katika mchezo wa leo, hali ambayo inadhihirisha mpambano utakua mkali na wa kuvutia.
Simba SC yenye alama 8 baada ya kushuka dimbani mara nne, inashika nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Namungo FC yenye alama 5 baada ya kushuka dimbani 4, ipo nafasi ya 11.