Makada Vijana wapatao 120 kutoka nchi sita zilizopo Kusini mwa Afrika wanashiriki mafunzo ya siku kumi katika Shule ya Uongozi Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoani Pwani ambayo yamezinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa Daniel Chongolo.
Akizungumza wakati ufunguzi huo hii leo Mei 25, 2022 Chongolo amesema mafunzo yatawajengea uwezo na kuwapa ari ya kuongoza ndani ya vyama vyao huku akiwataka kuendeleza misingi ya ujamaa na kujitegemea licha ya Dunia kuwepo katika utandawazi wa sayansi na teknolojia.
“Mafunzo haya kwa makada vijana ni muhimu hasa katika kuzungumza na kushauriana mambo ya msingi katika nchi zetu na yatasaidia kuwapa ari ya uongozi licha ya changamoto ya utandawazii katia Dunia,” amewaambia Chongolo.
Makada hao watapata fursa ya kutembelea iliyokuwa Kambi ya Wapigania Uhuru ya Mazimbu ili waweze kusoma vyema historia ya ukombozi kwa nchi zilizo Kusini mwa bara la Afrika itakayowasaidia kupata uhalisia wa kilichofanyika na viongozi waliotangulia.
“Tumieni fursa mtakayoipata hapa ipasavyo na hamna budi kuhakikisha nguvu kazi ya vijana inatumika katika uzalishaji kwenye nyanja ya sayansi na teknolojia na zaidi mtakapojionea historia ya wapiga uhuru pia mtapata kujua kazi kubwa iliyofanywa,” amesisitiza Chongolo.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa kundi la vijana Mkoa wa Pwani Khadija Khalid Ismail amesema wataendana na hali halisi ya kisasa kwakutumia utandawazi ili kupata mbinu za Uongozi bora.
Miongoni mwa vyama vinavyoshiriki mafunzo hayo yaliyodhaminiwa na Chama cha Kikomunisti Cha nchini China (CPC), ni ANC toka Afrika Kusini, FRELIMO cha Msumbiji, SWAPO – Namibia, ZANUPF – Zimbabwe, MPLA – Angola na wenyeji Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania.