Sakata la ofisi ya msajili wa vyama vya Siasa na chama cha NCCR-Mageuzi limechukua sura mpya baada ya James Mbatia kudai yeye bado ni Mwenyekiti halali wa chama hicho.

Kauli ya Mbatia inakuja ikiwa ni muda mfupi baada ya hii leo Mei 25, 2022, Msajili msaidizi wa vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza kusema wamemsimamisha James Mbatia na Sekretarieti yake kutojihusisha na siasa ndani ya NCCR.

Nyahoza alidai kikao cha Mei 21 mwaka huu cha kuwasimamisha Mbatia na sekretarieti yake kilikuwa ni halali na msajili alipokea taarifa kutoka kwa Katibu wa NCCR hivyo Mbatia hatakiwi kijihusisha na siasa ndani ya chama hicho.

Saa chache baadaye James Mbatia amezungumza na vyombo vya habari akidai kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za msajili wa vyama vya Siasa nchini yeye bado ni Mwenyekiti halali wa NCCR-Mageuzi.

“Narudia tena tunavyozungumza hivi sasa kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kwa mujibu wa sheria za vyama vya siasa na kwa mujibu wa katiba ya NCCR-Mageuzi mimi ni Mwenyekiti halali wa NCCR-Mageuzi,” amesisitiza Mbatia.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mwenyekiti wa azimio la kikao cha maamuzi Joseph Selasini Mei 21, 2022 alisema pamoja na kusimamishwa kwa Mwenyekiti huyo na wenzake pia wamelivunja Baraza la Wadhamini la NCCR  na kuteua wajumbe wapya hatua ambayo pia baadae ilipingwa na Mbatia.

Gwajima: Huu ni zaidi ya ukatili kwa watoto mitaani
Tanzania kuwapa shule ya uongozi Makada nchi 6