Jumla ya Watoto Milioni 152 wanatumikishwa Ulimwenguni kote, ambapo kati ya hao 25,803 sawa na asilimia 5.6 wapo katika ajira Visiwani Zanzibar wakiwa na umri kati ya miaka 5 hadi 17 walioajiriwa au kujiajiri.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa ya Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga katika maadhimisho ya siku ya kupambana na ajira za Watoto mjini Zanzibar.
Amesema kati ya watoto hao wa Visiwani humo, wakiume ni 15,855 na wa kike ni 9,948 wenye umri wa miaka 15 – 17 ambao wanaojishughulisha na ajira hizo, wengi wao hawajitambui kuliko wale walio na umri mdogo zaidi.
“Tafiti zilizofanyika watoto wenye umri wa miaka 15-17 ambao ni asilimia 21.7 ya watoto wanaojishughulisha na ajira za watoto Zanzibar, hii inabainisha kuwa idadi ya watoto wanaojitambua wanaofanya kazi ni kidogo sawa,” alisema Waziri huyo.
Waziri Soraga ameongeza kuwa, muongozo wa upinga unaonesha ajira za Watoto kwa Zanzibar zipo katika maeneo ya Kilimo, upandaji wa mwani, uvuvi, sekta ya utalii, ukahaba, ukataji matofali, kubanja kokoto na kazi za majumbani.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali katika suala la ajira za Watoto, hii ni pamoja na kuanzisha Sheria ya ajira nambari 11 ya mwaka 2005, Sheria ya mtoto nambari 6 ya mwaka 2011 na mikakati ya uwezeshwaji wa kiuchumi,” ameongeza Waziri Soraga.
Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na shirika la kazi Duniani (I.L.O), inakadiriwa watoto milioni 9 wataongezeka ulimwenguni kote katika ajira za utotoni ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.
Inadaiwa kuwa katika nchi za Africa, Ivory Coast na Ghana zina Watoto wengi walio na ajira za kilimo cha buni, huku Cameroon watoto kati ya miaka 7 mpaka 14 wakijishuhulisha na uuzaji wa biashara barabarani.