Kikosi cha KMC FC leo Jumanne (Juni 21) kimefanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuikabili Mbeya Kwanza FC katika mchezo wa Mzunguuko wa 28, utakaopigwa Kesho Jumatano (Juni 22), katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.

KMC FC itashuka dimbani Kesho, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba SC, iliyokua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Jumapili (Juni 19), kwa kukubali kichapo cha 3-1.

Msemaji wa KMC FC Christina Mwagala amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri kuelekea mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza FC, baada ya kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, ambao ulishuhudia wakitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Hassan Salum Kabunda.

“Kikosi chetu kipo katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa Kesho, kimefanya maandalizi yake ya mwisho leo Jumanne, tunatarajia kuwa na mchezo mzuri na wenye upinzani, japo tunaamini mambo yatatunyookea Kesho Jumatano.”

“Tunakubali tumepoteza mchezo wetu dhidi ya Simba SC kwa makosa ambayo Benchi la Ufundi limeshayafanyia kazi, hivyo sisi kama Uongozi na upande wa Mashabiki tunaamini makosa yaliyoonekana kwenye mchezo wa Simba SC Kesho yatakua faida kwa timu yetu.” Amesema Mwagala.

KMC FC ipo nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 32, huku Mbeya Kwanza FC inayoshiriki kwa mara ya kwanza ligi hiyo ikiwa nafasi ya 16 kwa kujikusanya alama 24.

Mbeya Kwanza FC matumaini kibao Ligi Kuu Tanzania Bara
Wizara yajipanga kuinua sekta ya TEHAMA Kimataifa