Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza FC Renatus Shija amesema hajakata tamaa na kikosi chake, licha ya kuendelea kuwa sehemu ya timu ambazo huenda zikashuka daraja mwishoni mwa msimu huu.

Mbeya Kwanza FC ambayo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu, imekua na muendelezo mbaya wa matokeo kwa siku za karibuni, hali ambayo imeendelea kuwaamishisha wadau wa Soka la Bongo kuwa, huenda ikashuka daraja.

Kocha Shija amesema amewaanda kisaikolojia wachezjai wake kuendelea kupambana hadi mwisho, huku wakiamini bado nafasi ya kusalia kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu ipo mikononi mwao, endapo watashinda michezo mitatu iliyosalia.

“Nimeshawaambia wachezaji wangu kuhusu umuhimu wa michezo inayotukabili kwa sasa, ni muhimu sana kushinda ili kujinusuru na janga la kushuka daraja, hatma ya kuibeba hii timu ipo mikononi mwao,”

“Nimewaambia hakuna linaloshindikana katika hii dunia, lakini bado nimewasisitiza kuwezekana huko kupo katika akili na kujituma kwao uwanjani na kuhakikisha wanashinda kwa kupata alama tatu.” Amesema Kocha Shija

Kuhusu mchezo wa Kesho dhidi ya KMC FC, kocha huyo amesema yupo tayari kwa kupambana na maandalizi aliyoyafanya, anaamini yatamuwezesha kufikia lengo la kupata alama tatu muhimu.

“Ninafahamu tunacheza ugenini, lakini hilo sio tatizo kwa sababu popote tunapaswa kupambana na kupata matokeo, wachezaji wangu wamejiandaa vizuri na wamenihakikishia kazi yao ni kwenda kupambana na kufikia lengo lililotuleta hapa Dar es salaam kwa ajili ya kupambana na KMC FC.”

Mbeya Kwanza FC inaburuza mkia wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 24, baada ya kucheza michezo 27, huku wenyeji wao KMC FC wakiwa nafasi ya 10 kwa kufikisha alama 32.

Barbara: Simba SC haijafeli usajili, tulieni mtaona
KMC FC yadhamiria jambo kwa Mbeya Kwanza FC