Nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.
Rai hiyo, imetolewa katika Kongamano la kwanza la siku ya Kiswahili Duniani lililoanza leo Julai 6, 2022 mjini Zanzibar, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Khamis Abdalla Saidi kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita.
Amesema, kuenea kwa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Mataifa mengine kunatoa ishara ua uwepo wa umuhimu wa kueneza lugha ya Kiswahili kama hatua mojawapo ya kufikia maendeleo katika nyanja mbalimbali Kimataifa.
Bosi mpya TPA akutana na gizo la siku saba
“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukifuatilia Kiswahili katika kila hatua na kutafuta na kubuni njia na mikakati ya muda mrefu na ya kisasa ya kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili,” amesema Bw. Saidi.
Ameongeza kuwa, Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kama bidhaa inayouzwa kwani ipo haja ya kuwekeza kwa kuwasomesha wataalamu wa lugha itakayoleta uwezo unaotakiwa katika kutoa huduma ya kufundisha, kutafrisi na kuandaa machapisho ya Kiswahili.
“Ni jukumu la vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kutilia mkazo mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti mbalimbali za lugha,” ameongeza Bw. Saidi.
Sakata la Katiba mpya, Viongozi upinzani wawekwa kizuizini
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa Lugha ya Kiswahili, ili kupata uzoefu wa matumizi yake na kujadili changamoto za lugha hiyo.
“Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili yataimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ni lugha ya biashara hivyo tunapaswa kujivunia lugha hii adhimu kwa maslahi mapana ya jumuiya yetu,” amesema Mhandisi Mlote.
Naye, Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Bi. Yusta Mganga amesema licha ya kuimarika kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki, bado hatua madhubuti zinahitajika ili kuhakikisha lugha hiyo inakuzwa na kuendelezwa.
“Kuna njia mbalimbali za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama vile kufanya tafiti, uandaaji wa makongamano na semina, katika kuandhimisha siku hii ni vyema tukatafakari mafanikio ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya yetu,” amesisitiza Bi. Mganga
Kongamano hilo, linalongozwa na Kauli Mbiu: “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” litahitimishwa kwenye siku ya Kilele cha Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, 2022.