Mtangazaji nyota, katika kituo cha televisheni cha Marekani cha Fox News amezua hasira nchini Kenya kwa kupendekeza kuwa wanawake wajawazito hawawezi kupiga kura katika nchi hiyo ya Afrika mashariki inayojiandaa kufanya uchaguzi.
Wakati wa mjadala kuhusu kipindi cha kejeli “Gutfeld”, mapema wiki hii, mtangazaji Emily Compagno alikosoa tweet ya mwimbaji wa Marekani Katy Perry, ambapo alisema kuhusu utoaji mimba.
“Vipi kuhusu Kenya, ambapo wanawake wajawazito hawawezi kuondoka majumbani mwao na kwa hivyo hawana haki kabisa ya kupiga kura,” Emily Compagno alijibu.
Video hiyo ya sekunde 29, ilisambaa nchini Kenya na kutawala mada zilizojadiliwa zaidi kwenye Twitter, huku watu mashuhuri wakishutumu maoni hayo.
“Taarifa hii si sahihi, inapotosha, inadhalilisha na inapaswa kuondolewa,” mchambuzi wa masuala ya kisiasa Pauline Njoroge alisema kwenye Twitter.
Esther Passaris, mbunge anayejulikana kwa msimamo wake kuhusu haki za wanawake, alikanusha wote wawili kwamba wanawake wajawazito hawawezi kuondoka nyumbani kwao na kwamba hawawezi kupiga kura.
“Wanawake wajawazito wana kipaumbele kwenye foleni (kwenye vituo vya kupigia kura). Wajawazito hujifungua bure Ondoa taarifa yako,” alitweet.
Kenya, itafanya uchaguzi wa urais, ubunge na mitaa Agosti 9, 2022 ambapo kwa sheria za nchi hiyo kila raia mtu mzima anaweza kusajiliwa kama mpiga kura na kupiga kura katika kila uchaguzi.