Hatimaye Uongozi wa Klabu ya Al Hilal ya Sudan umethibitisha kumpa Baraka zote Beki kutoka Ivory Coast Mohammed Ouattara, anayetajwa kusajiliwa na Simba SC.

Ouattara anatajwa kama mrithi wa Pascal Wawa aliyeondoka Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi kwa misimu minne mfululizo.

Mapema leo Jumatatu (Julai 18), Klabu ya Al Hilal imethibitisha taarifa za Beki huyo kuondoka klabuni hapo, na kumpa Baraka zote katika maisha yake mapya.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 23, ni pendekezo la Kocha wa sasa wa Simba SC Zoran Maki ambae alifanya nae kazi katika klabu za Wydad Casablanca (Morocco) na Al Hilal (Sudan).

Ouattara anatarajiwa kujiunga na Simba SC wakati wowote ndani ya juma hili, na huenda akaelekea Kambini Ismailia- Misri, moja kwa moja kuungana na wenzake.

Tayari Simba SC imeshakamilisha usajili wa wachezaji watatu wa Kimataifa na kuwatangaza hadharani ambao ni Moses Phiri (Zambia) Victor Akpan (Nigeria) na Augustine Okrah (Ghana).

Wazawa waliosajiliwa klabuni hapo hadi sasa wapo wawili ambao ni Nassoro Kapama na Habib Kyombo.

Vifo VVU vyapunguza kwa asilimia 50
Kocha Nabi: Sina haraka na KAMBI