Serikali, imesema kampeni iliyoandaliwa na GGM Kili Chalenge kwa ushirikiano wake na wadau, iimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa asilimia 50 kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene ameyasema hayo na kuongeza kuwa maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima, yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020 wakati maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.

Amesema, pamoja na mambo mengine Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa afua zinazotekelezwa za mwitikio wa VVU na UKIMWI zinaleta tija kwa makundi mbalimbali katika jamii nchini.

Waendesha Baiskeli katika kuhamasisha vita dhidi ya VVU na Ukimwi.

Simbachawene ameongeza kuwa, ili kufikia malengo katika kushinda vita hii dhidi ya VVU na UKIMWI, inahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wadau hasa sekta binafsi kwa kupata rasilimali fedha ya kutosha.

“Kili challenge inalenga kupunguza athari za kupungua kwa misaada ya wahisani na kuiwezesha nchi kuimarisha uwezo wa ndani kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI”

Awali, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimami miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema kampeni hiyo imepiga hatua tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene akimkabidhi Bendera mmoja wa washiriki wanaopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya VVU kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge 2022. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko.

Amesema kupitia kampeni ya hiyo, taasisi mbalimbali zimenufaika kwa kupata fedha za kutekeleza shughuli za mwitikio wa VVU na Ukimwi nchini ambapo mwaka 2020 Mfuko wa Kilimanjaro Challenge ulitoa shilingi milioni 800 kwa taasisi 20 zisizo za kiserikali.

“Tunawakaribisha sana wadau na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki katika kampeni hii na tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002,” amesema Shayo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko, alisema kwa muda wa miaka 20 tangu kampeni hiyo ianzishwe zaidi ya Shilingi 11 bilioni zimekusanywa na kusaidia katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene akiwa na wapandaji wa mlima Kilimanjaro.

Amesema, licha ya maendeleo mazuri yatokanayo na jitihada hizo, bado kuna maeneo ambayo yanahitajika nguvu zaidi ili kudhibiti VVU na UKIMWI na kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kama malengo ya Dunia yanavyoelekeza.

“Mojawapo ya malengo hayo ni kuzuia maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana kwani zaidi ya theluthi moja ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24, hususan vijana wa kike,” alisema.

Geita Gold Mine Limited (GGML), kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), ilianzisha zoezi hilo kwa lengo la kuchangia fedha za shughuli za udhibiti wa ukimwi ambapo ya wapanda mlima 52 walishiriki na wanatarajia kushuka Julai 21, 2022.

Kasi mabadiliko sheria za Habari yapungua
Al Hilal: Mohammed Ouattara RUHSA kuondoka