Madaktari na watoa huduma wa afya nchini, wametakiwa kuendelea kuwa na upendo, kujituma, kujitoa na kuzingatia weledi na maadili ya kazi zao.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango wakati akiongea na watoa huduma wa afya pamoja na wananchi wa Wilaya ya Siha.

Amesema, Serikali inatambua uwepo wa Wahudumu wa afya wanaofanya kazi zao kwa weledi, na kwamba wengi wao pia hupitia mazingira magumu na hatarishi ya utendaji.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango

“Mnafanya kazi ya Mungu na endeleeni kufanya hivyo bila kukata tamaa pamoja na Serikali kuendelea kuboresha maslahi yenu, nawasihi mtambue thamani ya masiha ya watu mnaowahudumia,” amesema Dkt. Mpango

Hata hivyo amewataka Madaktari na wahudumu wote wa afya nchini kutumia utaalamu wao na kutoa elimu ya afya na kinga kwa jamii ili kuleta uelewa.

Dkt. Mpango ameongeza kuwa, gharama za tiba kwa mtu aliyepata maambukizi ya ugonjwa ni kubwa na wakati mwingine hazibebeki kwa watanzania walio wengi hivyo Wizara ya Afya, madaktari na wahudumu waongeze jitihada za kutoa elimu ya afya.

Wahudumu wa Afya

“Kuweni wabunifu katika kutoa elimu, tumieni njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, teknolojia ya Habari na mawasiliano pamoja na mifumo ya kidigitali,” amefafanua Makamu wa Rais.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inapaswa kulenga katika kuwakinga watanzania na magonjwa ya kuambukiza na hata yasiyoambukiza ili kuepuka gharama kubwa za matibabu.

Kura isiyo siri kwa walemavu wa macho
Tanzania kinara 'EA' mionzi ya Dawa