Mgogoro wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT), ambao ulidumu kwa miaka sita umemalizika rasmi kufuatia Serikali kufanya uchunguzi na kubaini tuhuma zilizotolewa juu ya Viongozi Wakuu wa Kanisa hilo hazina mashiko.

Hayo, yamebainishwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT) Dkt. Abel Mwakipesile jijini Dodoma Julai 16, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za kanisa hilo.

Amesema, Serikali tayari imefanya kazi yake na kwamba kilichobaki ni kujenga umoja baina ya Vingozi na waumini ili kuendelea na kazi ya kulihubiri neno la Mungu kwa amani na upendo.

Majaliwa ‘amkubali’ mkandarasi Daraja la mawe

Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT), Dkt. Abel Mwakipesile.

Amesema, chanzo cha mgogoro huo ni aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa kanisa la EAGT, John Stephene Mahene kupinga kuondolewa madarakani baada ya kukiuka miongozo ya imani ya kanisa hilo, baada ya kuhoji ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa uliofanywa na viongozi wa kanisa.

“Tayari tumewaita kueleza mustakabali mzima wa mgogoro huo ambapo kutokana na maamuzi ya uongozi wa Msajili wa Jumuiya ulitoa barua yenye kumbukumbu Na.SA. 7183/PARTVI/50 ya tarehe 30Juni, 2022, ambayo ina maelezo ya kina,” amesema Askofu Mwakipesile.

Amesema, “Barua hiyo inaeleza jinsi Serikali ilivyofanya Uchunguzi wa kutosha na mwishowe ikabaini kwamba tuhuma zote walizotuhumiwa Viongozi Wakuu wa Kanisa la EAGT hazina msingi na wala Viongozi hao Wakuu hawahusiki kabisa na tuhuma zote.”

Waandishi wa Habari jijini Dodoma, wakiwa kazini wakati Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT) Dkt. Abel Mwakipesile akiongelea maamuzi ya Serikali juu ya kumalizika kwa mgogoro wa Kanisa hilo.

Aidha, Askofu huyo ameongeza kuwa mara baada ya vyombo vya Serikali kufanya uchunguzi wake na kujiridhisha kwa kina hakuna tuhuma zozote, hali hiyo imempa ujasiri wa kutangaza rasmi kumalizika kwa mgogoro huo pamoja na kutambua uongozi halali wa Kanisa la EAGT.

Hata hivyo, Dkt. Mwakipesile amesisitiza kuwa hatua hiyo imelisafisha Kanisa kufuatia mawazo potofu yaliyokuwa yanaenezwa juu ya uwepo wa mgawanyiko uliopelekea kuwepo kwa makundi mawili ndani ya EAGT.

“Maamuzi haya ya Serikali, yamefanya kikao cha Baraza la Waangalizi wa Kanisa la EAGT kilichokaa tarehe 12/07/2022 ambacho ndicho kikao chenye kauli ya mwisho ya kukata mashauri mbalimbali kuhusiana na Wachungaji kumshukuru sana Mungu pamoja na Serikali yetu kwa kutenda haki,” amebainisha Mwakipesile.

Kikao hicho kimewapa miezi mitatu kuanzia tarehe ya barua kuwa Mchungaji yeyote atakayetaka kurejea baada ya mgogoro kumalizika, atapokelewa na ngazi husika kwa sharti la kuandika barua kwa Uongozi kwamba ametambua kosa lake na sasa anaomba msamaha na kwamba yuko tayari kutumika chini ya Uongozi halali wa Kanisa la EAGT.

“Lakini kwa wale ambao watataka kuondoka EAGT, Baraza la Waangalizi limetamka kwamba lazima waheshimu Katiba yetu ya EAGT ya toleo la 2011 Ibara ya IX ambayo inasema, Mtumishi aachapo utumishi wake EAGT ataondoka pekee pasipo washirika wala mali za Kanisa,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Askofu Mwakipesile ametoa wito kwa kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022.

Vijana washauriwa kuchangamkia fursa za Kilimo
Majaliwa 'amkubali' mkandarasi Daraja la mawe