Vijana nchini, wametakiwa kujishughulisha ili kuandalia maisha yao ya baadaye kwa kuwekeza katika Kilimo ambacho ni biashara iliyopewa kipaumbele na Serikali ili kumkomboa mwananchi kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Usindikaji Mafuta ya Gilitu Enterprises Ltd ya Mjini Shinyanga, wakati wa ziara ya Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), ya kuwatembelea wadau wa Pamba kwenye baadhi ya mikoa inayolima zao la Pamba Kanda ya Ziwa.

Amesema, Serikali ipo karibu na wakulima kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo ambapo hivi karibuni umezinduliwa mfumo wa utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima na maafisa ugani wamepewa vitendea kazi ili kuhakikisha Kilimo kinatoa ajira kwa vijana na kukuza pato la nchi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Usindikaji Mafuta ya Gilitu Enterprises Ltd, Gilitu Makula akionesha jinsi mafuta ya alizeti yanavyozalishwa katika kiwanda Mjini Shinyanga.

“Vijana msing’ang’anie tu kukaa mjini, wekezeni kwenye kilimo njia ni nyeupe serikali imetupa nguvu katika kilimo. Naomba turudi kijijini tukalime, twendeni tukaanzishe hata kilimo cha umwagiliaji kwani kilimo ni biashara na kinalipa,” amesema Makula.

Makula amesema, “Vijana msiwe waoga wa kuthubutu, jaribuni kufanya kila kitu badala ya kulia lia kuwa hakuna ajira ingieni kwenye kilimo, wenye mitaji wekezeni kwenye kilimo Rais Samia yuko bega kwa bega na wakulima na tunaye Waziri wa Kilimo Hussein Bashe atatusaidia.”

Makula amesema ili nchi ipate maendeleo ni lazima kuwe na viwanda vilivyo na malighafi ili kuwa na uzalishaji endelevu wa bidhaa zitakazosaidia kuinua pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.

Gilitu Makula akionesha mafuta ya alizeti yaliyosindikwa katika ujazo tofauti tayari kwa kuingia sokoni.

“Ili nchi yetu ipate uchumi tunahitaji viwanda viwe vingi hivyo vijana wanapaswa kuchangamkia fursa katika kilimo ili viwanda hivi vilivyopo vipate mali ghafi mfano hapa nina kiwanda lakini malighafi hazitoshi kufanya uzalishaji wa mafuta ya pamba na alizeti,” amebainisha.

Aidha, amewataka wananchi wakiwemo vijana kulima zao la pamba na alizeti kwa tija ili kupata mazao mengi hali itakayosaidia kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta nchini.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaasa vijana kuacha kuchanganya biashara na starehe na tamaa ya kutaka kufanikiwa kwa njia za mkato bali wawe na wivu wa mafanikio kwa kumtanguliza Mungu mbele.

MSD yakabidhi vifaa tiba kituo cha Afya
Serikali yamaliza mgogoro wa muda mrefu EAGT