Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeteua timu ya wataalamu wabobezi wa Habari watakaotoa mafunzo kwa waandishi wa Habari za mchakato wa mabadiliko ya sheria za Habari nchini.

Jukwaa hilo limefanya kikao na wanataaluma washauri wa waandishi hao wa Habari Julai 15, 2022 likiwa na lengo la kuweka mikakati itakayosaidia kufikia malengo kusudiwa.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ndiye aliyeongoza kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Balile amesema lengo la uteuzi wa timu hiyo unalenga kuongeza chachu ya harakati kuelekea mabadiliko Sheria za Habari nchini.

“Tunapaswa kuwa na waandishi wabobezi katika harakati hizi, ndio maana tumeunda timu ya wanataaluma ambao watawasimamia waandishi,” amesema Balile.

Aidha, Balile ameongeza kuwa, “Mimi kama mwenyekiti naamini, timu hii ya wataalamu wabobezi, itasaidia kwa kiwango kikubwa kunyoosha mwelekeo na hatimaye kupata matokeo chanya.”

Wanataaluma walioteuliwa kusimamia waandishi hao ni pamoja na Mhariri wa Raia Mwema, Joseph Kulangwa, Mhariri wa Majira, Stella Aron, Mhariri wa Mwananchi Rashidi Kejo, na Angela Akilimali ambaye ni Mhariri wa TBC.

Buckreef, mfano ajira kwa wazawa
Mpango afungua Maabara ya Afya ya Jamii Siha