Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kufikisha huduma mbalimbali za jamii zikiwemo za afya kwa wananchi wote hadi waishio maeneo ya vijijini ili wazipate kwa wakati.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Julai 16, 2022 wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Mtoa iliyopo Wilayani Iramba Mkoani Singida baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha afya cha Mtoa.

Amesema, kukamilika kwa kituo hicho kutawawezesha wananchi hao kupata huduma za afya zikiwemo za maabara, mama na mtoto na upasuaji karibu na makazi yao na kusema Rais Samia ameelekeza huduma za afya ziwafikie wananchi wote hadi waishio vijijini.

“Wilaya ya Iramba, Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya sita kwa lengo la kusogeza huduma hizo karibu na makazi ya wananchi na Rais wetu mama Samia anataka huduma za afya ziwafikie wananchi wote,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, Majaliwa ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Iramba kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mtoa, ambapo ameiagiza Wizara ya Fedha ya Mipango kupeleka kiasi cha shilingi milioni 262, 635,689 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

Mpango afungua Maabara ya Afya ya Jamii Siha
Afya bora kipaumbele cha Serikali: Simbachawene