Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha maeneo ya Shule zote za Msingi na Sekondari yanapimwa na kupatiwa hatimiliki.

Waziri Bashungwa, ametoa agizo hilo Julai 15, 2022 katika ziara aliyoifanya Shule ya Sekondari Ndama iliyopo Wilaya ya Karagwe, na kubaini shule hiyo kutokuwa na hatimiliki hali inayosababisha kuwapo kwa uvamizi wa maeneo kwa shule na taasisi za Serikali.

“Nawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Shule zote za Msingi na Sekondari nchini nzima zinapimwa na kuwa na hati ya maeneo yake,” amesema Waziri Bashungwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, akiwa katika moja ya majukumu yake ya kikazi.

Amesema, baada ya kusikiliza changamoto za Shule hiyo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/23, itapeleka fedha za kujenga maabara ya Baiolojia na Fizikia katika shule hiyo, ili wanafunzi wasome kwa vitendo.

Aidha, katika hatua nyingine Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, kupeleka Shilingi Milioni 30 zilizokuwa zimetengwa na Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa maabara, ili fedha hizo zitumike kujenga jengo la utawala katika Shule hiyo.

Agizo hilo linaambatana na la kutenga fedha na kuweka kipaumbele cha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule hiyo, kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri na kusisitiza halmashauri zote nchini kutekeleza maagizo hayo.

Mwananchi akisukuma mkokoteni wa maji.

Waziri huyo, pia amemuagiza Meneja wa mradi wa maji mjini (BUWASA), Wilaya ya Karagwe kuhakikisha mabomba ya mradi wa maji unaotekelezwa katika Mji Mdogo wa Kayanga, yanafikishwa kwenye shule hiyo ili kuondoa changamoto ya utafutaji maji nje ya eneo la shule kwa Wanafunzi.

Milioni 662 kukamilisha kituo cha afya Mtoa
Wanahabari wapewa darasa sheria ya Habari