Ili kuwawezesha Wanahabari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa marekebisho ya sheria za vyombo vya habari nchini, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA TAN), na Shirika la Kimataifa la Kuwezesha Vyombo vya Habari (IMS), imeendesha semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi hao Mkoani Lindi

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jesse Kwayu amesema wanahabari hao wanatakiwa kushiriki na kutoa mapendekezo yatakayoboresha vifungu korofi vya sheria ya Habari ili kupata sheria yenye vipengele rafiki kwa tasnia ya habari nchini.

“Kwa kuzifahamu sheria mtaweza kuwa mstari wa mbele kujadiliana changamoto mbalimbali za sheria hizi kwani hakuna mtu atakuja kutoka nje kuzungumzia changamoto unazokumbana nazo. Wewe ndiye unayeumizwa na hizi sheria na ndiye mwenye jukumu la kutafuta njia ya kuzitatua,” amefafanua Kwayu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jesse Kwayu.

Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo wameishukuru MISA TAN kwa kuwaongezea ujuzi wa kuzifahamu vyema sheria za habari nchini, hali itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Kupitia semina hii tumenufaika sana kujua vifungu kandamizi vya sheria mbalimbali ikiwemo EPOCA na Sheria ya Huduma ya Habari. Uwezo tuliojengewa utatuwezesha kushiriki kikamilifu katika zoezi la maboresho ya sheria hizi,” amesema mmoja wa washiriki.

Wakiwa katika semina hiyo wanahabari wamepitia na kujadili vipengele mbalimbali vya Sheria vinavyokandamiza uhuru wa vyombo vya habari kwa kujieleza na haki ya kupata taarifa.

Wanahabari Kazini.

Semina hiyo ni nimuendelezo wa jitihada za MISA TAN kwa kushirikiana na IMS ya kuwafunda wanahabari kuzifahamu sheria zinazoongoza tasnia ya habari nchini, ambapo zaidi ya Wanahabari 30 wameshiriki na kunufaika nayo.

Serikali kuhakiki maeneo ya shule na kuyapa hatimiliki
DC akemea watoto kufanya biashara, ataka waende shule