Watu wawili, wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa na Polisi Mkoani Kigoma, wakituhumiwa kuhusika na tukio la uporaji kwa kutumia Bunduki katika soko la kijiji cha Bukirilo wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa Kigoma, Menrad Sindano, amesema tukio hilo lililotokea Julai 21, 2022 majira ya saa mbili usiku katika Kijiji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Burundi huku akisema majambazi waliouawa wanadaiwa kuwa ni raia wa Burundi.
Amesema, katika tukio hilo majambazi watatu walikuwa wakitumia Silaha aina ya AKA 47 na walipora vitu mbalimbali ikiwemo vitenge, simu na pesa taslimu katika maduka matatu ya Dawa, Vitenge na kibanda cha hufuma za fedha.
Majambazi hao, wametambulikwa kwa majina ya Harelimana Ananias (30) na Nimpangalitse Jean (36), mara baada ya kupekuliwa katika nguo ambapo vilikutwa vitambulisho viwili na kuonesha marehemu walikuwa ni raia wakazi wa mkoa Ruyigi nchini Burundi.
“Wananchi waliripoti tukio hilo kituo cha Polisi Gwanumpu wakiomba msaada baada ya kuwazingira majambazi hao wakiwarushia mawe, ndipo askari Polisi na Jeshi kutoka kikosi cha mpakani cha Bukirilo walifika eneo la tukio na kuanza kurushiana risasi na majambazi wawili kujeruhiwa vibaya na mmoja alifanikiwa kukimbia,” amesema Kaimu Kamanda.
Majambazi haa waliojeruhiwa, Kwa mujibu wa Sindano amesema walifariki wakiwa njiani wakipelekwa hospitali ya Wilaya ya Kakonko, na kudai kuwa msako unaendelea kumtafuta jambazi mmoja aliyekimbia.
Aidha, amesema walifanikiwa kukamata bunduki moja aina ya AKA 47 ikiwa na magazine mbili, risasi 15, maganda matatu ya risasi, simu tisa walizokuwa wamepora na fedha taslimu shilingi 82,000.