Tathmini iliyofanywa na Jeshi la Polisi nchini, imeonesha asilimia 80 ya matukio ya ajali za Barabarani huchangiwa na makosa ya kibinadamu kwa kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi kinyume na sheria.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini aliyoitoa kwa waandishi wa Habari Julai 22, 2022 nakuongeza kuwa makosa hayo ya kibinadamu pia husababisha ajali kutokana na Dereva kuyapita magari mengine bila tahadhari.

“Tathmini hiyo pia imeonesha Madereva huendesha huku wakitumia simu zao za mikononi, kuendesha wakiwa wamelewa, kukosa umakini na kubeba idadi kubwa ya abiria kuliko uwezo wa Gari kitu ambacho ni hatari,” amefafanua Naibu Waziri.

Muonejako wa gari iliyopata ajali mbaya ya barabarani.

Amesema, katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na matukio ya ajali za barabarani zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali hasa katika mikoa ya Iringa, Simiyu na Kagera.

Hata hivyo Sagini amesema tayari ajali hizo zimefanyiwa uchunguzi na katua mbalimbali za kisheria zilichukuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usalama Barabarani na kuwataka wamiliki wa vyombo vya moto vya usafirishaji kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya leseni za Usafirishaji nchini.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea na msako wa kukamata magari yanayokiuka sheria za usalama barabarani kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria madereva wake ambao wamekuwa kisababishi cha ajali nyingi zisizo na lazima.

Taarifa ukatili wa kijinsia kusajiliwa rasmi
Mradi 'ishi vizuri' wazaa matunda uraiani