Asasi za kiraia kisiwani Pemba, zimeweka mpango na mkakati wa pamoja wa kufuatilia rasirimali za Umma katika jamii, utakaosaidia kuongeza uwajibikaji wa taasisi za umma katika kusimamia rasilimali hizo kwa maendeleo ya nchi.
Wakizungumza katika mkutano wa kujadili mbinu bora za ushawishi na utetezi katika ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi, wamesema lengo jingine la kuwepo kwa mfumo huo ni kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kwenye uongozi.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Omar Khamis amesema kuwepo kwa mpango wa pamoja wa ushawishi na utetezi kwa asasi za kiraia utasaidia kukabili kwa pamoja changamoto zinazokwaza wanawake kupata haki zao.
“Suala la ushawishi na utetezi kwenye ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi katika jamii tunaweza kulifanikisha kwa kuweka mkakati wa pamoja ambao utatusaidia kujua changamoto na kuzitaftia ufumbuzi kwa pamoja kuliko kila taasisi kusimama kivyake,” amesema Khamis.
Mwakilishi kutoka Jumuiya ya Mwamvuli wa Asasi za kiraia Pemba (PACSO), Stara Sifuni amesema, mjadala huo umefungua ukurasa mpya kwa asasi za kiraia kuwa na uwezo wa kufuatilia na kuiwezesha jamii kutambua rasilimali zote ambazo ni muhimu kwa maendeleo yao.
Stara amesema, “Wengi tulikuwa hatuujui mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya umma (PETS) lakini baada ya taaluma hii tutaitumia kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kusaidia jamii kuwa na ufahamu wa kutosha na hatimae kuondokana na urasimu wa rasilimali za umma ambazo hupelekea kuwakosesha wanajamii haki zao za msingi.”
Kwa upande wake mratibu wa TAMWA-ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said amehimiza asasi za kiraia kuongeza jitihada za kutambua mbinu muhimu za uchambuzi wa matatizo ya kijamii hasa za uongozi kwa wanawake ili ziwawezeshe kuandaa mipango sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kushirikiana na jamii.
“Kuna umuhimu mkubwa sana kwa asasi za kiraia kutambua mbinu muhimu za uchambuzi wa matatizo ya kijamii katika ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya uongozi, na hii itatusaidia kujua ukubwa, udogo, uzito, sababu na madhara yake katika jamii,” amefafanua Fat-hiya Mussa Said.
Awali, Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema jamii ina haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika upatikanaji wa haki kwenye matumizi ya rasilimali za umma Ili kuweza kufikia malengo ya kuijenga nchi kwa pamoja.
Mradi huo wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi (SWIL), unatekelezwa Visiwani Zanzibar na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO), na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.