Mawaziri wa Nishati kutoka Nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi kwa pamoja wameazimia kumpitisha Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba kuwa Mwenyekiti wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Rusumo Hydropower.
Mawaziri hao, wamefikia azimio hilo mara baada ya kufika na kukagua hatua mbalimbali zilizofikiwa na mradi huo unaohusisha nchi hizo tatu, ambapo baadaye walifanya kikao cha ndani na kufikia maazimio hayo.
Kikao hicho, kiliwahusisha Mawaziri hao watatu ambao ni Waziri wa Nishati Rwanda, Dr. Eng. Ernest Nsabimana, Waziri wa Nishati wa Burundi, Uwizeye Ibrahim na Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba ambaye anarithi uongozi huo kutoka kwa Waziri wa Nishati wa Rwanda.
Miongoni mwa majukumu ya Mwenyekiti mpya, January Makamba ni pamoja na kuitisha na kuongoza vikao vyote vinavyohusu mradi huu wa Rusumo Hydropower, pamoja na kuratibu mawasiliano yote yanaohusiana na mradi huo.
Mara baada ya Makabidhiano hayo Waziri Makamba ameongea na Wanahabari kuzungumzia kuhusu hali ya mradi huo kwa kusema kasi ya ujenzi inaendelea vizuri na hadi kufikia sasa uko kwenye asilimia 95.
Amesema, “Mradi ukikamilika Kampuni hii itayauzia umeme mashirika ya Umeme kwenye hizi nchi tatu (Rwanda, Burundi na Tanzania) na mradi huu umefadhiliwa na wafadhili wa Benki ya maendeleo ya Afrika na wafadhiri wengine wa Maendeleo.”
Aidha, Waziri Makamba amebainisha kuwa, “Tunautegemea mradi huu kuongeza uhakika wa umeme kwenye ukanda huu wa Ziwa Victoria, jawabu la matatizo yote ya umeme katika kanda ya Ziwa ni mradi huu.”
Mradi wa Rusumo Hydropower, unatatarajia kumalizika Novemba 2022 ukihusisha nchi tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2023, Wananchi tayari watakua wameanza kunufaika.